iTEC
Wanafunzi Ngurdoto walipolipuka kufurahia ugeni wa umeme Sola (Written by Swahili language)

 

(This article is written by Swahili language)

Ni ugeni ambao una tafsiri ya moja kwa moja, kusaidia kwa kiasi kikubwa kufundishia somo la Tehema, ambalo hivi sasa lipo kwenye mtaala wa elimu ya shule za msingi.
Ni hatua itakayiwezesha kuinua kiwango cha uelewa wa wanafunzi kuhusu somo hilo la Tehema ambalo hivi sasa linatumika katika nchi mbalimbali duniani katika masuala ya mawasiliano, pia kusukuma maji ya kisima kwa matumizi shuleni.
Matarajio yaliyoko ni kwamba, utatumika kufundishia watoto shuleni kwa matumizi ya projekta, pia kunufaisha wananchi kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya kujiongezea kipato, kusikiliza radio, kuangalia TV na kupata taarifa mbalimbali duniani kupitia vyombo hivyo vya habari.

Neema umeme
Akizungumza na Nipashe, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ngurdoto, Neema Urio, anasema unapotaja kijiji cha Ngurdoto, hakifahamiki kwa wengi.
Anafafanua kwamba, kijiji cha Ngurdoto kipo kata ya Maji ya Chai na kilianzishwa mwaka 1973 ambapo mpaka sasa kina vitongoji vitano vyenye wakazi 4000.
Kwa muda wa miaka 45, wananchi waliishi kwenye giza la kukosa umeme na walitegemea mbadala wa vijinga vya moto, vibatari na tochi katika kupata mwanga wa matumizi ya nishati nyumbani na watoto kujisomea.

Mwalimu Mkuu
Mwalimu Mkuu anasema, hivi sasa hali ya maisha ya wananchi kijijini imeanza kubadilika, wananchi wako furahani, hasa wanafunzi baada ya Serikali ya Korea Kusini, kupitia Kituo cha Ubunifu wa Tekinolojia na Nishati (ITEC), kimejenga kituo cha kuzalisha umeme wa nishati ya jua, ili kuboresha sekta ya elimu, afya na kusaidia wananchi kuanzisha shughuli za kujiongezea mapato, hali inayoelezwa kuwa mafanikio makubwa ya miaka 45 sasa.
“Ninaishukuru sana Serikali ya Korea kupitia ITEC kuleta mradi huu katika kijiji cha Ngurdoto, kwa sababu wanafunzi watatumia umeme huu kujisomea na kuongeza ufaulu zaidi .
“Itasaidia ofisi za walimu na madarasa ya wanafunzi kuwa na umeme, lakini pia walimu watatumia umeme huo kujifunza compyuta ili waweze kuzitumia kufundishia wanafunzi darasani”, anasema.
Pia ameiomba serikali ya Korea Kusini kupitia ITEC na Serikali ya kijiji, iwasaidie kufikisha umeme huu shuleni ili kutumia kupampu maji ya kisima kwa matumizi ya kupikia, kunywa, chooni na kadhalika.
Pia, wanawaomba wafadhili hao kuwasaidia kupata kompyuta walau 30, ili wanafunzi wajifunze Tehema kwa vitendo, mtaala unaofunzwa kuanzia darasa la tatu hadi la tano.
Anasema, somo la sayansi na teknolojia linahitaji kompyuta na ujenzi wa vyumba viwili vya vyenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 30, ili wanafunzi wengi wanufaike.
Mpaka sasa Shule ya Msingi Ngurdoto, ina wanafunzi 800, walimu 17 na kuna mwalimu mmoja mahsusi kwa kompyuta na vyumba 14 vya madarasa.
Mwalimu Urio anasema, pia wanahitaji madarasa matatu kwa ajili ya wanafunzi, vyumba viwili vya kompyuta na mwalimu wa kompyuta wa kuwafundisha walimu wengine.

Changamoto
Mwalimu Mkuu anasema, katika mfumo wa maji yanayosukumwa kutoka umeme wa chanzo cha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Hata hivyo, Mwalimu analalamika katika chanzo hicho cha maji katika Shule ya Msingi Ngurdoto, bado kuna tatizo kubwa kwa sababu wazazi hawatoi pesa za kununua uniti za umeme, ambayo ni kuchangia Sh. 100 kwa mwaka.
“Hivi sasa hali imebadilika sana, wazazi hawatoi hela kabisa, hivi sasa natumia fedha za familia yangu kununua uniti za umeme.
“Kwa mwezi natumia zaidi ya Sh.10,000 ili wanafunzi waendelee kupata maji. Nafikiri upatikanaji wa umeme wa nishati ya jua, utasaidia kupunguza gharama hapa shuleni,” anasema.
Anasema, pamoja na kuwapo kisima, bado maji yanayopatikana hayatoshelezi matumizi ya shule, kwa sababu ni kisima cha kuvuna maji ya mvua wakati wa kiangazi na siyo cha kuchimba.
“Tunavuna maji ya mvua kutoka kwenye mabati, yanaenda moja kwa moja kwenye kisima na tunatumia dawa ili kuua vijidudu na maji yake salama kwa matumizi ya wanafunzi na walimu,” anasema.

Mwanafunzi mhitimu
Grory Lyimo ni mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne mwaka jana, katika Shule ya Sekondari Ngurdoto, anautafsiri hiyo ni mabadiliko makubwa katika mazingira ya kimasomo anayoyajua.
“Kutokanana na matumizi ya vibatari macho yalikuwa yanauma na saa nyingine kifua kinauma na nilikuwa natumia ‘lisaa limoja’ tu kujisomea.
“Sasa hivi tunamshukuru Mungu, katika kijiji chetu hali imebadilika, wanafunzi wanajisomea vizuri na kila mtu anatembea barabarani bila woga, kwa sababu taa zinawaka kila mahali. Wananchi wamenunua friji wanataka kuanzisha biashara za ‘ice cream’ kwenda kuuza shuleni”, anasema.

Kituo ITEC
Mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Ubunifu wa Tekinolojia na Nishati (ITEC), DK. Herb Rhee, anasema kituo kina uwezo wa kuzalisha kilowati 6.5 za umeme na mpaka sasa kuna jumla ya nyumba 43 katika kitongoji cha Mseseweni zimeunganishiwa umeme huo.
Hiyo ni kwa ajili ya matumizi majumbani na shughuli nyingine za kujiongezea kipato pamoja na taa 10 za usalama barabarani usiku.
Ili kuufanya mradi endelevu, kijiji kimeunda kamati ya kukusanya fedha kutoka kwa wananchi kulingana na matumizi yao ya umeme na zitasimamiwa na kamati iliyoteuliwa na serikali ya kijiji, chini ya ITEC.
“Mradi huu utakabidhiwa Serikali ya Kijiji cha Ngurdoto. Fedha zote zitakazokusanywa na kamati, zitatumika kumlipa meneja wa Kituo kwa ajili ya kuendeshea mtambo na kufanya matengenezo, kama kutatokea hitilafu yoyote kwenye mtambo na matengenezo mengine,” anasema.
Vile vile ITEC itaendelea kuunganisha umeme bure katika nyumba nyingine na fedha za matumizi ya umeme zitatozwa na kamati kulingana na matumizi ya kila nyumba kila mwezi. Aidha ITEC kitaendelea kufunga smart mita kwa ajili ya kufuatilia matumizi ya umeme kila nyumba.
Hiki ni kituo cha pili kujengwa na ITEC, kituo cha kwanza kilijengwa katika kijiji cha Mkalama kilichopo kata ya Masama-Rundugai wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro na jumla ya nyumba 50 kijijini mkalama ziliunganishwa umeme huo.
Aliwaomba wananchi wa kijiji cha Ngurdoto hasa kitongoji cha Mseseweni kutumia umeme huo kupambana na umasikini na kusaidia watoto kusoma katika mazingira mazuri.
“Ebu shangilieni upatikanaji wa umeme wa jua katika kijiji chenu, huu ni mwanzo, pamoja tunaweza kufanya vitu vingi vya kuleta maendeleo katika kijiji chetu na vijiji jirani, tukiwa pamoja hakuna kitu kisichowezekana,” anasema.

Mwenyekiti Kijiji
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngurdoto, Moses Ayo, anasema kilianzishwa mwaka 1973 na sasa kina wakazi 4,000 ikiwa na vitongoji vitano anayovitaja ni: Bondeni, Mburiashi, kati, Msamaneni na Mseseweni.
“Tunamshukuru Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kukubali mradi huu kuwepo katika kijiji chetu, hasa kitongoji cha Mseseweni na serikali ya Korea kumtuma DK.Rhee kuja kuona hali tuliyokuwa nayo hapa kijijini, ambayo imesababisha leo kijiji chetu kupata umeme wa nishati ya jua,” anasema
“DK.Rhee alipokuja kijijini, alitukuta tupo kwenye giza na leo hii wananchi wamepata umeme, jumla ya nyumba 43 tayari zimeunganishwa na umeme wa nishati ya Jua,” anafafanua
Mwenyekiti kijiji anaendelea kuwa ujio wa umeme huo wa jua ni hatua moja, bado wanahitaji umeme wa Tanesco kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kwa sababu mahitaji ni makubwa kijijini hapo na umeme umeshafika katika kitongoji kimoja tu, kati ya vitano.

DC Arumeru
Naye mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro, anaishukuru serikali ya Korea Kusini, kusaidia wananchi wa kitongoji cha Mseseweni kupata umeme wa nishati ya jua.
“Hii ni hatua nzuri ambayo imefanywa na serikali ya Korea Kusini katika kuunga juhudi za Mheshimiwa Rais Awamu ya Tano, Rais John Magufuli, katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi,” anasema.
“Nitoe wito kwa uongozi wa kijiji, mradi huu umetokana na kodi za wananchi kutoka Korea Kusini, tumieni mradi huu kuondokana na umasikini, mhakikishe mradi unawanufaisha,” anasisitiza.
Kupitia mradi huu watoto watakuwa wanasoma katika mazingira mazuri yenye mwanga wa kutosha na kuongeza ufaulu shuleni.
“Nitoe wito, kamati nyingi zinashindwa kufanya kazi kwa sababu ya majungu na mambo ya kisiasa. Wekeni siasa pembeni, siasa iliyo safi ni ile inayoondoa changamoto za wananchi.
“Hatutaki siasa katika mradi huu, hizi ni fedha za moto, ukila zitakutumbua na mimi nitafuatilia ukusanyaji wa fedha hizi na kila anayepata umeme apewe risiti,’ anawatahadharisha

 

Nipashe. 2019. 03. 05

https://www.ippmedia.com/sw/makala/wanafunzi-ngurdoto-walipolipuka-kufurahia-ugeni-wa-umeme-sola

915 | 06-03-2019